Umuhimu wa 'Aqeedah
Na: Sheikh 'Abdul-'Azeez al-Qaaree
Asili: Manhaj ya Salafi
Imefasiriwa Na: Abufarida Muhammad A. Basawad

Bismillaahir Rahmaanir Raheem

Mtume Muhammad (Sallallahu 'alyhi wasallam) alimwambia Mu'aadh bin Jabal alipokuwa katika safari ya kuelekea Yemen: "Unakwenda kwa watu walio miongoni mwa watu wa Kitaab. Itakubidi ulinganizi wako wa kwanza kwao uwe ni wa kumuabudu Mwenyezi Mungu. Iwapo watamkubali Mwenyezi Mungu, basi wapashe habari yakwamba Mwenyezi Mungu Amewafaridhia juu yao, Swala tano katika nyakati zao za asubuhi na mchana." [al-Bukhari na Muslim]

Hadeeth hii iko wazi. Haihitaji wingi wa maelezo. Mtume (Sallallahu 'alyhi wasallam) aliitekeleza kanuni hii katika harakati zake za ulinganizi wa Da'wah katika Uislamu. Aliishi Makkah kwa muda wa miaka kumi na tatu, akiwafunza na kuwaelimisha maswahaba zake kuhusiana na Imaan na urekebishaji wa itikadi walizokuwa nazo. Hayo ndiyo malezi waliyo-lelewa nayo maswahaba.

Amesema Jundub ibn 'Abdullah al-bajaly, "Tumejifunza Imaan (kuamini), kisha tukajifunza Qur'aan ambayo (nayo) ikatuongezea Imaan yetu." Nae 'Abdullah ibn 'Umar akasema: "Sisi tuliishi kwenye zama za wakati ambapo mmoja wetu aliipata Imaan mwanzo kabla hajaipata Qur'aan, na pindi Sura zilipokuwa zikiteremshwa tulikuwa tukijifunza maamrisho na makatazo yake na mambo yaliyohalalishwa na kuharamishwa na jinsi ya kukabiliana nayo. Lakini nimewaona watu wengi miongoni mwao walikuwa wanapewa Qur'aan kabla ya Imaan na akaisoma kuanzia mwanzo wake hadi mwisho wake asijue maamrisho wala makatazo yake - bila ya kuwa na mazingatio yoyote ya hiyo Qur'aan. Mfano wake ni kama mtu aliezitupilia mbali tende zake (usomaji wake wa Qur'aan haumfaidishi na chochote)."

Hii ndiyo desturi ambayo Mtume Muhammad (Sallallahu 'alyhi wasallam) aliyo-walelea nayo maswahaba zake: Imaan mwanzo na kisha Qur'aan. Hii inalingana na alivyoeleza Imaam Abu Hanifah: "Kuifahamu dini mwanzo (Tawheed) na kisha kuyafahamu ma'alumati yake (ya kisheria)." Imaan ni sharuti zitakaswe mwanzo na baadae ifuate miradi mengine ya dini. Akasema nae Imaam ash-Shafi'i, "Mja yoyote atakaemuona Mwenyezi Mungu na dhambi za aina yoyote, isipokuwa shirk, ni bora kuliko kuonana Nae (Mwenyezi Mungu) hali ya kuwa juu ya Imani za uzushi."

Katika lugha ya kiarabu, neno 'Aqeedah limetokamana na neno 'aqadah. Kilugha (kiarabu) mtu anaweza kusema "'Aqada Kamba" ikiwa kamba imekazwa madhubuti. Na, "'Aqada bei" au Amekubaliana nae bei, ikiwa mtu ameafikiana na kuandikishiana mkataba kuhusu mapatano yao ya kibiashara. Na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa ta'aalah) akasema katika Qur'an, (kama ilivyofasiriwa) "Na wale mliofungamana nao ahadi wapeni sehemu yao ('Aqadat)" [Surat An-Nisaa (4):33]. Na pia Akasema tena Mwenyezi Mungu, (kama ilivyofasiriwa) "Lakini atakukamateni kwa viapo mlivyoapa na nia mlioifunga barabara ('Aaqadtum)" [Al-Maidah (5):89]. Aya hizi zinamaanisha uthibitisho na mafungamano na kitu fulani kama ilivyobainishwa kwenye aya isemayo, (kama ilivyofasiriwa) "Na timizeni ahadi mnazozitoa kwa jina la Mwenyezi Mungu mnapoahidi wala msivunje hizo ahadi baada ya kuzithubutisha hali mumekwisha mfanya Mwenyezi Mungu kuwa Shahidi wenu. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua (yote) mnayoyafanya." Mtu akisema, "Aqadtu kadhaa na kadhaa," maana yake moyo wake umethubutu juu ya kadhaa na kadhaa.

Kwahivyo 'Aqeedah au I'tiqaad kulingana na wanavyuoni wa ki-islamu ni: Imani thabiti iliyotulia juu ya moyo wa mtu pasi na kusita-sita au shaka yoyote. Haihusiki na dhana yoyote, shaka au tuhuma.

Imaam Abu Hanifa akaiita ilimu hii iliyo pana kwa jina la Fiqh-ul-Akbar ("Ufahamu Mkubwa") ambayo ndilo shina la kuifahamu dini hii. Na akayaita maarifa ya kisheria (Shar'), ujuzi wa kitaalamu. Wanavyuoni wengi wa kiislamu hutumia neno Tawheed kwa kila kinacho-fungamana na kuamini. Hii ni kwa sababu jambo muhimu zaidi hapa ni msingi wa Tawheed ulio kwenye matamshi ya, "Hapana apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah."

Kulingana na wao, Tawheed imegawanyika sehemu mbili: Tawheed ya kusadiki na kukiri na Tawheed ya makusudio na matendo. Tawheed ya kusadiki na kukiri ni Tawheed ya Upweke wa Mu-umba na Tawheed ya Majina Yake na Sifa Zake (hapana mshirika katika Uumba wake na ni Pekee katika majina Yake na Sifa Zake). Tawheed ya makusudio na matendo ni Tawheed ya Uola au kuwa hapana apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah (Yeye ndie wa Pekee anaestahiki kuabudiwa kwa haki). Jee, katika Qur'aan, mas-ala haya yameitwa kwa jina gani?

Qur'aan imeyataja mas-ala haya makubwa kwa jina la "Imaan". akasema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa-Ta'aalah) (kama ilivyofasiriwa): "Na namana hivi tumekufunulia wewe (Muhammad) wahyi kwa amri yetu. Ulikuwa hujui Kitaab ni nini wala Imaan; Lakini tumefanya kitabu hiki (Qur'aan) ni nuru, ambayo kwa nuru hiyo Tunamuongoza Tumtakae..." [Ash-Shura :52]

Ukurasa wa Pili

1