Umuhimu wa 'Aqeedah
Na: Sheikh 'Abdul-'Azeez al-Qaaree
Asili: Manhaj ya Salafi
Imefasiriwa Na: Abufarida Muhammad A. Basawad

Bismillaahir Rahmaanir Raheem

Hapana shaka yoyote yakwamba nyoyo za waumini ni lazima ziwe thabiti juu ya "nguzo za Imaan". Na mtu yoyote hatoitwa mu'min kwa kujua na kufahamu nguzo hizo peke yake, lakini mpaka afikie daraja ambayo atakuwa anakiri (anakubali) na kutekeleza yanayompasa kama ilivyo-elezwa katika hadeeth ya Jibreel. Kwahivyo Imaan katika hali hii imo ndani ya duara la Uislamu. Lau kama Imaan ni kuijua haki kwenye nyoyo tu, basi Shetani na Fir'auni pia wangelikuwa ni waumini [Alikuwa Shetani akimtambua Mwenyezi Mungu kuwa n Mola wake, lakini aliangamizwa kwa ajili ya kiburi chake na wivu. Na Fir'auni nae, hata kama alidai Uungu, alikuwa anatambua yakwamba Mola ni Mwenyezi Mungu na pia hapana anaestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu. Akatueleza Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa-Ta'aalah) katika Qur'aan (kama ilivyofasiriwa): "Akasema (Musa): 'Bila shaka umekwishajua kuwa hakuna alieteremsha (hoja) hizi isipokuwa Mola wa Mbingu na Ardhi, kuwa dalili; (ila unajibabaisha tu)...'" [al-Israa':102] Hata kama waliijua haki, lakini hawakuitekeleza kwa kuzielekeza 'ibaadah zao kwa Mwenyezi Mungu peke Yake].

Katika hadeeth ya Jibreel, Mtume (Sallallahu 'alyhi wasallam) alizifafanua nguzo za Imaan hii ambazo inampasa kila kiumbe kuziamini alipoulizwa, "Ni nini Imaan?", akasema: "Ni kuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika Wake, na Vitabu vyake, na Mitume Wake, na siku ya mwisho na kuamini Qadar (kheri yake na shari yake)." Ni lazima juu ya kila mtu kuzijua nguzo hizi n akuzielewa kisawasawa na kuwa na Imani nazo kama walivyoamini na kuzielewa maswahaba wa Mtume (Sallallahu 'alyhi wasallam) na wafuasi wao. Vilevile wanahusika humo ma-Imamu wanne, Sufyaan ath-Thawree, Sufyaan ibn-'Uyaynah, 'Abdullah ibn al-Mubaarak na wengine kama hao na pia Muhammad ibn Ismaa'eel al-Bukhaari, Muslim ibn al-Hajjaaj, Sheikh ul-Islaam ibn Taymiyyah na al-Haafidh ibn al-Qayyim. Na wanavyuoni kama hao ambao waliofuata mwenendo huohuo wa kuziamini nguzo hizo.

Huu ndio wajibu wa kwanza alokabidhiwa mwana-adamu. Hapana ikhtilafu ya maoni juu ya suala hili miongoni mwa wanavyuoni ambao rai zao zinastahili kufuatwa. Akasema Imaam Abu Haneefah, "Kuifahamu (Ujuzi wa) Imani ni bora kuliko kuyafahamu maarifa ya kisheria." Katika msemo huo aliikusudia Imani kuwa ni Tawheed na maarifa ya kisheria kuwa ni Hukmu za Kisheria. Akatanguliza kuifahamu Tawheed kabla ya kuzifahamu Hukmu za kisheria. Nae Sheikh al-Islaam al Haruwi al-Ansaaree (f.481 AH) akanukuu katika awali ya kitabu chake, I'tiqaad ahl-as-Sunnah, "Wajibu wa kwanza unaompasa mja ni kumtambua Mwenyezi Mungu. Jambo hili limethubutu kutokamana na Hadeeth ya Mu'aadh alipoambiwa na Mtume (Sallallahu 'alyhi wasallam): "Unakwenda kwa watu walio miongoni mwa watu wa Kitaab. Itakubidi ulinganizi wako wa kwanza kwao uwe ni wa kumuabudu Mwenyezi Mungu. Iwapo watamkubali Mwenyezi Mungu, basi wapashe habari yakwamba Mwenyezi Mungu Amewafaridhia juu yao, Swala tano katika nyakati zao za asubuhi na mchana...".

Kutoka katika chimbuko hili, wakatangulia wanavyuoni mashuhuri wa ki-Islamu. Hebu jaribu kuzingatia alivyofanya Imaam Muhammad ibn Ismaeel al-Bukhaaree katika kitabu chake "al-Jaami' as-Saheeh", ambacho ni kitabu bora zaidi kilicho saheeh baada ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu (al-Qur'aan). Utashangaa jinsi Mwenyezi Mungu Alivyompa maarifa na Hikma nyingi katika kuifahamu dini. Imaam huyu mashuhuri, ameanzia kitabu chake na mlango wa "Mwanzo wa wahyi", kisha akafuatiliza na milango ya Imaan na baadae Ilimu. Ni kama alikuwa akituashiria, Mwenyezi Mungu Amrehemu, kwa kutujulisha yakuwa wajibu wa kwanza juu ya mwana-adamu ni Imaan (au kuamini), na haipatikani Imaan hiyo isipokuwa kwa ilimu. Na asili ya Imaan na ilimu ni wahyi (uteremsho). Akaanza kwa kutuonyesha vipi wahyi ulivyoteremshwa na baada ya hapo akazitaja Imaan na ilimu. Mipango hiyo haikuzuka tu kwa ajali bali pana mazingatio makubwa ndani yake.

Haya ni jumla ya tulokusudia kuwadokeza na kwa ajili hiyo, tunazipaza sauti zetu. Mas-ala ya 'Aqeedah ni yenye kutangulizwa. Imani na ilimu ni njia za kuifikia. Na asili ya ilimu na Imani ni Kitaab (Qur'aan) na Sunnah.

1