
Kuna maafikiano makubwa baina ya Ahlus-Sunnah wal-Jamaa'ah kuwa ni wajibu wetu kushikamana na Jamaa'ah na kuwa imekatazwa kujitenga nayo; Kushikamana na Jamaa'ah ni jambo jema na kujiepusha na kujitenga nayo ni ufisadi.
Kuna dalili nyingi kutoka katika Qur'aan na Sunnah ambayo imetaja kuhusu jambo hili, mpaka kufikilia kiwango cha kuwa tawaatur. Vile vile kuna riwaya chungu nzima kutoka kwa ma salaf (watangulizi wetu wema) kuhusiana na haya. Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata'aalah) Akasema: "Na mushikamane na Kamba ya Mwenyezi Mungu, nyote kwa pamoja, wale musifarikiane" (Surat- Aal-Imraan 3:103)
Ibn Abee Haatim[2] amesema: "Babangu alinieleza kuwa: Amr Ibn 'Alee As-Sairafee alinieleza, akisema: Abdu Rabbihi Ibn Baariq al-Hanafee - na akamsifu kwa uzuri - kuwa alinihadithia na kusema: Simaak Ibn al-Waleed al-Hanafee amesema yakuwa alikutana na Ibn 'Abbaas mjini al-Madinah na akamwambia:"Wasemaje kuhusu huyu kiongozi wetu anayetutawala, na kutunyanyasa (kutudhulumu na kutukandamiza) na kutushtumu, jee ni kwa nini basi tusimzuie (yaani tumpige vita na kumpinga)?"
Ibn Abbas akamjibu:"Laa! bali mumtii, Ewe Hanafee". Na akaendelea kusema: "Ewe Hanafee, (shikamana na ) Jamaa'ah, Jamaa'ah! Kwa hakika mataifa yalio watangulia waliangamizwa kwa ajili ya kujigawanya (kufarikiana wao kwa wao). Jee hukusikia Mwenyezi Mungu aliposema: "Na mushikamane na Kamba ya Mwenyezi Mungu, nyote kwa pamoja, wala musifarikiane...."
Amesema Ibn 'Atiyyah katika tafseer yake [3], "Rai za wanavyuoni wa tafseer zimetofautiana kuhusu maana ya hii sehemu ya ayah "Kamba ya Mwenyezi Mungu". Basi Ibn Mas'ood akasema "Kamba ya Mwenyezi Mungu (ina maanisha) ni Jamaa'ah". Anas Ibn Malik anatueleza kuwa mtume wa Mwenyezi Mungu (Salallahu 'alayhi wasallam) amesema: "Kwa hakika banu Israeel waligawanyika mapote sabiini na moja . Ummah wangu utagawanyika mapote sabiini na mbili - yote hayo ni yenye kuangamia katika (moto wa) Jahannam isipokuwa moja. (Maswahaba) wakamuuliza:"Ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu, ni kundi gani litakalo okoka?" Naye akakunja ngumi na kusema;"Jamaa'ah", halafu akawasomea aya "Na mushikamane na Kamba ya Mwenyezi Mungu, nyote kwa pamoja" [4].
Ibn Mas'ood alisema katika moja ya khutbah zake:"Nyinyi nyote kwa ujumla, munawajibika kuwa watiifu (kwa Allah) pamoja na Jamaa'ah, kwani hii ndiyo Kamba ya Allah aliotuamrisha sisi Mola wetu."
Qataada naye akasema:"Kamba ya Allah ambayo Ametuamrisha tushikamane nayo ni Qur'aan".
Nae As-Suddee akasema: "Maana ya Kamba ya Allah ni kitabu chake Mwenyezi Mungu". Ibn Mas'ood na Ad-Dahhaak pia walisema hivyo. Na mengine mengi pia yalisemwa ambayo yamefanana na haya (katika misemo iliotangulia).
Neno "jamee'an" (nyote kwa pamoja) imeungana na amri " 'I'tasimoo" (shikamaneni), basi maana yake itakuwa "muwe wamoja juu ya kushikamana na hiyo Kamba ya Allah". Na "musifarikiane" ina lenga aina ya migawanyo ambayo haitawafanya mushiriki katika Jihaad na mambo ya kulinda dini na Neno la Mwenyezi Mungu. Huu ndiwo mgawanyiko uliotokamana na fitna na kutokubaliana katika mambo ya imani." [mwisho wa maneno ya Ibn 'Atiyyah]
Nami nasema kuwa, kutofautiana katika tafseer ya "Kamba ya Allah" ni tofauti inayo tuashiria aina nyingi ya maana ya neno hilo, wala sio tofauti ya maana halisi ya neno hilo, kama tulivyoelezwa na Ibn 'Atiyyah, Ibn 'Abdil-Barr na muhaqqiqeen wengineo. Na maoni yake kuwa (Kamba ya Mwenyezi Mungu) inamaanisha Kitabu chake inakusanya misemo yote ya salaf. [5]
Al Qurtubee alitaja katika tafseer yake [6], rai ya wale wanaosema "Kamba ya Allah" inamaanisha Qur'aan, na rai ya wale wanaosema kuwa inamaanisha Jamaa'ah. Kisha akasema:"Maana iliyokusudiwa hapa zimekaribiana na zimefanana kwani Mwenyezi Mungu anatuamrisha tuwe wamoja na kutukataza na kufarikiana. Hii ni kuwa (huko) kufarikiana ni maangamizi na kushirikiana na Jamaa'ah ni maokovu.
Naye Shaykhul Islaam ibn Taymiyyah akasema: "Kamba ya Mwenyezi Mungu" imefasiriwa kuwa; Kitabu Chake, Dini Yake, Uislamu, Dhati, Amri Yake, Agano Lake, Utiifu kwa Allah, na Jamaa'ah. Misemo yote haya yametajwa na maswahaba na wale waliowafuata katika kutenda mema mpaka siku ya Kiyama. Na yote haya ni Saheeh, kwani Qur'aan inatuamrisha juu ya Dini ya Uislamu - na hii ndiyo Amri ya Mwenyezi Mungu, (vile vile ndilo) Agano lake na Utiifu wa Mola. Na kushikamana na yote haya kwa ujumla (kwa umoja wa watu) haitawezekana isipokuwa kwa Jamaa'ah. Na dini ya Uislamu ki uhakika na kuwa mkweli na wazi kwa Mwenyezi Mungu.
Ibn Jareer at-Tabaree amesema katika tafseer yake [8] kuwa Qataada amesema kuhusu aya hii "Wala musifarikiane, na mukumbuke baraka ya Mwenyezi Mungu juu yenu" - Kwa hakika, Mwenyezi Mungu anachukia kuona kuwa ummah umegawanyika na Anatukataza na jambo hili. Na anapenda kuona tunatwi'i na kushikamana na Jamaa'ah. Basi pendaneni baina yenu kwa yale Mwenyezi Mungu anayowapendelea - kiasi cha uwezo wenu. Na hamna nguvu isipokuwa kwa (amri yake) Mwenyezi Mungu.
Kumbukumbu
1. Neno la mfasiri: Jamaah inakusudia ummah wa waislamu kwa ujumla walioshirikiana juu ya haki au juu ya mambo ya utawala wa ummah.
2. Tafseer ya Ibn Hateem (2/455) na aliye nukuu hadithi hii ni Abd Rabihh Ibn Baariq al-Hanafee. Al-Haafidh Ibn Hajar asema kumhusu mtu huyu:"Yeye ni mwaminifu lakini hufanya makosa (wakati wa kunukuu)"
3. Al-Muharra al-Wajeez fee Tafseer al-Kitaab-il-Azeez (3/182) (Iliochapishwa na al-Maghrib)
4. Imenukuliwa na Ibn Jareer katika Tafseer yake (4/32), Ibn Haatim katika tafseer yake (2/452-453) kutoka kwa njia ya Yazeed ar-Raqaashee kutokamana na Anas, lakini silsila huo ni dhaifu. Hii hadithi imetolewa kupitia njia nyingi zenginezo kutoka kwa Anas na wengineo. Misemo yote haya tofauti huongeza nguvu baina ya hii hadith, isipokuwa haikutajwa miongoni mwa yote haya kutaja aya, isipokuwa hii riwaya moja tu ya Anas - kulingana na ninavyo elewa.
5. Kuna kauli sita ambazo Ibn al-Jawzee amezitaja katika Tafseer ya Zaad al-Maseer (1/432) (Imechapishwa na al-Maktab al-Islamee)
6. Al-Jaami' Li-Ahkaam-il-Qura'an (4/159) (Imechapishwa na Dar Al-Kutub)
7. Minhaaj as-Sunnah (5/134) (Imechapishwa na Jaamiah al-Imaam Muhammad Ibn Sa'ood al-Islamiyyah)
8. Jaami' al-Bayaan 'an Ta'weel Ayy-il-Qur'aan (4/32)
|