Kujitolea Muhanga (Suicide Bombing) Katika Mizani ya Wanavyuoni wa Ahlul-Sunnah
Imefasiriwa Na: Abu-Farida Muhammad Awadh Basawad

Bismillaahir Rahmaanir Raheem

Wanavyuoni wazungumzia kuhusu utekaji nyara na kujiuwa (kujitolea muhanga - "Suicide Bombing")

Mukhtasari wa waraka huu umetolewa kwa min-ajil ya kuusambaza msimamo halisi wa Uislamu na watu wa Sunnah dhidi ya upotofu wa wale wanaojuzisha umwagaji wa damu kwa njia isiyofaa.

Pote la watu wanaounga mkono vitendo kama hivyo lilianza kujitokeza kwenye karne za mwanzo za Uislamu na likahusika pote ndilo na mauaji ya halaiki ya Maswahaba wa Mtume (Sallallaahu alayhi wasallam). Ikawa tangu wakati huwo hawakukoma vitendo vyao hivyo viovu na wakadhihirika na ujinga wao katika kila zama. Inawapasa Waislamu kuvitambua vitimbi vyao na kujiepusha na mfumo wao unaokwenda kinyume na mafundisho ya Qur'aan, Sunnah, na Maswahaba.

(Tafadhali soma na usambaze ujumbe huu)

Bismillaah wal-Hamdulillaah was-salaatu wassalaam 'ala Rasoolillaah; Waba'd...

1. Alivyosema Imaam Ibn Uthaymeen (Rahimahullaah) kuhusiana na milipuko ya wanaojitolea muhanga huko Palestine na sehemu nyengine ulimwenguni.

Imaam Ibn Uthaymeen (Rahimahullaah) amesema katika mafunzo ya Riyaadh-us-Saaliheen (1/165-166), pindi alipokuwa akizieleza faida zipatikanazo kwenye hadeeth ya Suhayb, Radhi Zake Allaah zimshukie:

Yakwamba, Rasoolullaah (Sallallaahu alayhi wasallam) amesema, "Palikuwepo na mfalme miongoni mwa wale waliokuja kabla yenu, nae alikuwa na mchawi. Basi hali ya uzee ilipomjilia (yule mchawi) akamwambia mfalme, 'Mimi sasa nishakuwa mkongwe, kwahivyo niletee mimi kijana ili nimfunze kazi hii ya uchawi'..." hadeeth ikaendelea. (Angalia Riyaadh-us-Saaliheen, no.30 kwa ukamilifu)

Jambo la nne: Inaruhusiwa kwa mtu kujitolea kwenye hali ya hatari kwa jambo litakalo kuufaidisha ummah wa kiislamu, kwa sababu yule kijana alimuonyesha mfalme jinsi ambayo atakavyoweza kumu-uwa, jambo ambalo litakalomletea kifo chake. Nalo (jambo lenyewe) ni achukuwe mshale kutoka kwenye podo lake (mkoba wa kubebea mishale)... n.k

Akasema Shaykh-ul-Islaam (Ibn Taymiyyah), "Kwavile hii ilikuwa ni Jihaad katika njia ya Allaah, iliyosababisha ummah mzima huwo kuamini kihakika, nae hatahivyo hakupoteza chochote, kwani ingawaje yeye alikufa, alikuwa hana budi yakwamba atakufa tu pindi utakapotimia muda wake."

Amma kuhusu kile wanachofanya baadhi ya watu kuhusiana na kujitolea muhanga, wakajitatiza miili yao kwa baruti na mizinga kisha wakawakurubia ma-Kuffaar na kujilipuwa nao, basi hii hukmu ya kujiuwa - Tunamuomba Allaah Atunusuru. Kwa yeyote atakaejiuwa basi atakuwa mtu huyo ni wa motoni milele, abakie humo milele, kama ilivyo kwenye hadeeth ya Mtume (Sallallaahu alayhi wasallam), "Na yeyote atakaejiuwa kwa silaha ya chuma, basi silaha hiyo ya chuma itabakia mkononi mwake, na ataendelea kujidunga matumbo yake akiwa ndani ya moto wa Jahannam milele na milele."
(Imepokewa na Imaam al-Bukhaaree, na.5778 na Muslim na.109, katika kitabu cha Eemaan).

Sasa, kwa vile mtu huyu amejiuwa mwenyewe na akawa hakuufaidisha Uislamu na chochote. Anapojiuwa mwenyewe na watu wengine kumi, au mia moja, au na watu wengine mia mbili, basi Uislamu hautofaidika na jambo hilo, kwani watu hawatosilimu, kinyume cha vile alivyofanya yule kijana. Yule adui atazidi kufanya ukatili wake, na kitendo hicho kitazidi kuchochea uadui na uchungu ndani ya moyo wake hadi ifike katika kiwango cha kutaka kulipiza kisasi cha maangamizi dhidi ya Waislamu.

Hili ndilo jambo linalopatikana kutokana na vitendo vya Mayahudi na watu wa Palestine ikawa mmoja wa Wapalestina anajilipuwa yeye mwenyewe na kuwauwa watu wengine sita au saba, na kisasi chake ikawa wanawauwa sitini au zaidi. Jambo kama hili halileti mafanikio yoyote kwa Waislamu, na wala hawanufaiki nalo wale ambao waliokuwemo ndani ya milipuko hiyo.

Misimamo yetu katika matukio kama hayo ni kwamba wale watu wenye kujitolea muhanga (milipuko) wamejiuwa kwa kujidhulumu nafsi zao, na hapana shaka yakwamba watauingia moto wa Jahannam, Tunamuomba Allaah Atulinde na kwamba watu kama hao si Ma-Shaheed. Lakini hatahivyo, iwapo mtu amefanya kitendo hicho kutokana na ufahamu wa ki-makosa, na kudhania yakwamba kitendo hicho ni cha sawa au inafaa, basi tunatumainia yakwamba ataokolewa kutoka katika madhambi hayo, lakini ama kuhusu awe miongoni mwa ma-Shaheed, haiwezekani kwa vile hakuiandama njia ya Ma-shaheed. Lakini mtu yeyote afanyae ijtihaad na akakosea, atalipwa thawabu moja (ikiwa yeye anastahiki kufanya hiyo ijtihaad)."

[Mwisho wa maneno ya Shaykh]
-----------------------------------------------------------------------
2. Imaam Ibn Baaz (Rahimahullaah) kuhusiana na utekaji nyara wa ndege na kushika mateka.

Kutokana na yale yanayojulikana na kila mtu hata mwenye chembe ya fahamu zake ni kwamba utekaji nyara wa ndege na kushika mateka watoto na mengine kama hayo ni uhalifu wa hali ya juu, kote ulimwenguni. Maafa ya uovu huwo ni makubwa na yenye kuenea, kama yalivyo makubwa madhara yake na udhia anaofanyiwa mtu asie na hatia; jumla ya maafa ambayo hakuna awezae kuyafahamu isipokuwa Allaah.

Vilevile, kutokana na yale yanayojulikana ni kwamba uhalifu huu hauhusu nchi fulani juu ya nchi nyengine, wala haihusu kikundi fulani juu ya kikundi chengine, bali ni ulimwengu mzima kwa ujumla.

Hapana shaka kuhusu maafa ya uhalifu huu; kwahivyo ni juu ya kila Serikali na wale wenye majukumu miongoni mwa Wanavyuoni na wasiokuwa wao kuyapa mas-ala haya umuhimu sana, na kuyakemea maovu hayo vikali kabisa."

Shaykh Ibn Baaz
Kayfa Nu'aalij Waaqi'unaa al-Aleem - Uk. 108-109
-----------------------------------------------------------------------
3. Utekaji nyara wa Ndege na Meli.

Suali: Kuna baadhi ya watu ambao huteka nyara Ndege au Meli, na hufanya hivyo ili kuitenza nguvu nchi ambayo Ndege hiyo au Meli hiyo inapoelekea. Pana uwezekano wa kutishia kuwauwa abiria, na wakati mwengine pia huwa-uwa baadhi ya abiria, mpaka matakwa yao yasikilizwe. Sasa ni nini hukmu kuhusian an vitendo kama hivyo, kwani vitendo kama hivyo huwatisha abiria?

Jawabu: Ni juu ya (kila) nchi kuwa na ulinzi imara ili kupambana na mifano ya watekaji kama hawa kutokana na kuziteka nyara (Ndege na Meli). Ni wajibu wa (kila) nchi kuwapa mashirika yote ya Ndege, walinzi (wakiwa katika nchi zao), ambao wenye uwezo wa kupambana na maarifa yoyote ya utekaji utakaofanywa magaidi; kama vile ambavyo wanavyosimama imara kuwafanyia ukaguzi abiria wote kabla ya kuingia ndani ya Ndege. Hivyobasi, na wasimruhusu yoyote kuingia ndani ya Ndege mpaka wahakikishe yakwamba hakuna yeyote mwenye silaha hata kama ni kipande cha chuma. Zaidi ya hayo yote, baadhi ya vikosi vyengine vya wahalifu huilazimisha Ndege kubadilisha njia yake ili waelekee mahali kwengine, sasa iwapo atapatikana (baadhi ya abiria au wafanyi kazi wa Ndege) mwenye afya na nguvu za ki-mwili awezae kuwatenza nguvu, basi mipango ya maharamia hao itaangamizwa.

Kwahivyo hapana shaka yakwamba utekaji nyara ni jambo la makosa, ujinga na upotofu. Na zaid, ni kitendo cha uhalifu kupindukia mipaka kunakosababisha tisho kwa abiria, na kuwatia khofu kwa jambo ambalo wasilokuwa na nguvu nalo, na Allaah Yanamuelea yote hayo."

Shaykh Ibn Jibreen
Kayfa Nu'aalij Waaqi'unaa al-Aleem - Uk.113
-----------------------------------------------------------------------
4. Imaam Ibn Uthaymeen kuhusiana na Kuwavamia maadui kwa kujilipua nao ndani ya Magari.

Suali: Ni nini hukmu kuhusu vitendo vya Jihaad kwa njia ya kujiuwa, kama vile kulitatiza gari kwa baruti na mizinga kisha kujivurumiza kwa maadui, ambapo mtu anajua bila ya shaka yoyote yakwamba matokeo yake ni kifo?

Jawabu: Kwa hakika maoni yangu ni kwamba yeye atakuwa ni mtu aliye jiuwa mwenyewe (amefanya kitendo cha kujiuwa), na matokeo yake ni kuadhibiwa motoni, kutokana na usaheeh uliopokewa kutoka kwa Mtume (Sallallaahu alayhi wasallam).

[(Kwa hakika, mtu yeyote atakaejiuwa (kwa kukusudia), basi hapa shaka yakwamba ata-adhibiwa ndani ya moto wa Jahannam, ambapo ataishi humo milele)]
[Bukhaaree (5778) na Muslim (109 na 110)].

Hatahivyo, kwa yule aliye mjinga na asiejua, na akachukulia kuwa kitendo chake ni kizuri na chenye kumridhisha Allaah (Subhaanahu wata'aalah), basi tunatarajia yakwamba Allaah (Subhaanahu wata'aalah) amsamehe kwa yale ambayo aliyoyafanya kutoka na (ujinga) wa Ijtihaad. Hata hivyo, sioni msamaha kwake kwenye hizi zama zetu. Hii ni kwa sababu kitendo hichi cha kujitolea muhanga kinajulikana mno na kimeenea miongoni mwa watu, kwahivyo inawapasa watu kuwauliza wenye ilimu (Wanavyuoni - Scholars) kuhusiana na kitendo hicho, mpaka njia ya uongofu ibainishwe kutokamana na njia ya kimakosa.

Jambo la kushangaza ni kwamba, hawa watu hujiuwa wenyewe haliyakuwa Allaah (Subhaanahu wata'aalah) Ameshalikataza jambo hilo, kama Alivyosema kulingana na tafsiri ya maneno yake (Subhaanahu wata'aalah):

"Wala msijiue, Hakika Allaah ni mwenye kukuhurumieni." [Soorah An-Nisaa 4:29]

Na watu wengi miongoni mwao hawatamani chochote isipokuwa kuwalipa kisasi maadui, kwa njia yoyote itakayokuwa, iwe halaal au haraam. Kwahivyo matamaniwa yao ni kujitosheleza kiu yao kwa kulipa kisasi.

Tunamuomba Allaah Atubariki kwa kuona mbali katika Dini Yake na vitendo vyenye kumridhisha Yeye, kwa hakika Yeye ndie Mwenye nguvu juu ya kila kitu.

Imaam Ibn Uthaymeen
Kayfa Nu'aalij Waaqi'unaa al-Aleem - Uk.119
-----------------------------------------------------------------------
5. Imaam Ibn Uthaymeen kuhusiana na hukmu ya kujiuwa (kujitolea muhanga).

Suali: Ni nini hukmu kuhusu kujiuwa katika Uislamu?

Jawabu: Kujiuwa, ni mtu anapojiuwa mwenyewe kwa kukusudia kwa kutumia njia yoyote. Jambo hili ni Haraam na ni miongoni mwa madhambi makubwa, na pia imekusudiwa katika maneno (yenye maana iliyo pana) ya Allaah (Subhaanahu wata'aalah):

"Na mwenye kumuwa Muislamu kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannam, humo atakaa milele; Na Allaah amemghadhibikia na amemlaani na amemuandalia adhabu kubwa." [Soorah An-Nisaa 4:93]

Na ikathibitishwa katika Sunnah kutoka kwa Mtume Muhammad (Sallallaahu 'alayhi wasallam) yakwamba amesema:

Kwa hakika, mtu yeyote atakaejiuwa (kwa kukusudia), basi hapana shaka yakwamba ata-adhibiwa ndani ya moto wa Jahannam, ambapo ataishi humo milele)]
[Bukhaaree (5778) na Muslim (109 na 110)].

Ukweli ni kwamba, yule anaefanya kitendo cha kujiuwa, sana hufanya hivyo kutokana na hali iliyomkabili ya kukata tamaa, emma kutokana na matokeo ya moja kwa moja kutokana na Amri ya Allaah au vitendo vya wana-adamu. Ndipo utakapomuona akishindwa kulistahamilia jambo ambalo lililomsibu, na hali yake inakuwa ni mfano wa yule aitishae msaada haliyakuwa yumo ndani ya jekejeke la moto. Kwahivyo amejiendeleza kutoka katika lile lililo zito (jambo baya) kuelekea kwenye lile lililo ovu zaidi. Na lau kama angalikuwa na subira, basi Allaah angelimsaidia katika kupambana na yaliyo mazito.

Imaam Ibn Uthaymeen
Kayfa Nu'aalij Waaqi'unaa al-Aleem - Uk.120
-----------------------------------------------------------------------
6. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (F. 728)

Ma-Khawaarij ni wale ambao wenye kuhalalisha damu iliyoharamishwa. Wao huwafanya Waislamu kuwa ni makafiri kutokana na madhambi wanayoyafanya. Wanawafanya viongozi wote Waislamu kuwa makafiri na wakaitisha watu kufanya mapinduzi na kuasi na kumwaga damu.

Amesema Mtume (Sallallaahu 'alayhi wasallam): "(Ma-Khawaarij) ni majibwa wa Jahannam" (Musnad Ibn Abee Awfaa, Dhilaal-ul-Jannah Fee Takhreej Ahaadeeth as-Sittah).

Akasema Mtume (Sallallaahu 'alayhi wasallam): "Lau kama ningaliishi katika wakati wao, ningeliwachinja kwa kichinjo cha Aad (taifa zima lililotajwa na Allaah katika Qur'aan ambalo aliloliangamiza kutokana na Uovu wao)." [Bukhaaree na Muslim]

Akasema Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah,

"Na njia, seerah, ya Waislamu haikukoma kuwepo juu ya mfumo (njia) huu. Wao hawakuwafanya (yaani: Khawaarij) kuwa si Waislamu kama wale aliwopigana nao As-Siddeeq (Radhiallaahu 'anhu). Na jambo hili , licha ya maamrisho kutoka kwa Mtume (Sallallaahu 'alayhi wasallam) kupigana nao, kama ilivyo kwenye hadeeth iliyo saheeh, na pia licha ya yale yaliyopokewa kuwahusu wao katika hadeeth ya Abu Umaamah, na kupokewa na At-Tirmidhee na wengineo [*] yakwamba wao ni "waovu zaidi wa wale waliowahi ku-uwawa chini ya mbingu na ni jambo lililoje bora kwa yule mwenye ku-uwawa na wao". Kwa maana yakwamba wao ni wenye kuwadhuru Waislamu zaidi kuliko wengine, kwani hapana wanaowadhuru Waislamu kuliko wao, si Mayahudi wala Manasara. Kwani wao wanajitahidi kumuuwa kila Muislamu ambae asokubaliana na maoni yao, kuhalalisha damu za Waislamu, mali zao, na kuwachinja watoto wao, na huku wakiwafanyia Takfeer. Na kwa jambo hilo, wakidhania kuwa ni Ibaadah, kutokana na ujinga wao na uzushi wao uliowafanya kupotea."

Minhaj-us-Sunnah 5/248.
[*] Imesahihishwa na Imaam al-Albaanee (Rahimahullaah) katika Saheeh Sunan at-Tirmidhee (na. 2398)
-----------------------------------------------------------------------
7. Imaam Ibn Baaz kuhusiana na wale wenye kushiriki katika Ulipuwaji mabomu, utekaji nyara...

Suali:(Ni nini hukmu) kuwahusu Jamaa'at-ul-Jihaad (kikundi chenye kutekeleza majukumu ya kulipuwa mabomu na vitisho na vitendo vyengine viovu) na kushirikiana nao?

Jawabu: "... na haifai kushirikiana nao, wala wasipewe salaam. Bali, inafaa kujitenga nao, na watu wanapaswa kuonywa kuhusu maovu yao. Kwani wao ni Fitnah kubwa (mtihani/msiba) na ni wenye kuwadhuru Waislamu, na ni ndugu zao mashetani!"

[Kutoka katika Kaseti (na.11), iliyorekodiwa katika mwezi wa Dhul-Hijjah 1408H (1987 CE) at-Tawiyyatul-Islaamiyyah].