Jee, Isomwapo Qur'aan twafaa kuzungumza?
Imetayarishwa Na: Sameh Strauch
Asili: Mafaaheem Khaati'ah 'An Ba'dh al-Aayaat al-Qur'aaniyyah wal Ahaadeeth an-Nabaweeyyah
Imefasiriwa Na: Abufarida Muhammad A. Basawad

Bismillaahir Rahmaanir Raheem

Kuhusiana na maneno ya Allaah (Subhaanahu wata'aalah) (kama yalivyofasiriwa):

"Na isomwapo Qur'aan isikilizeni na nyamazeni ili mpate kurehemewa" [Surat al-A'raaf 7:204]

Kwa Waislamu wengi, kutokana na aya hii, imeharamishwa kuzungumza katika mahali ambapo pana mtu anaisoma Qur'aan; Lakini, Ibn Katheer asema: "Maana yake ni ukiwa ndani ya Swala ya Jamaa'ah, pindi Imamu anaposoma kwa sauti (swala za Alfajiri, Maghrib na 'Ishaa') kama ilivyopokewa na Imaam Muslim kwenye Saheeh yake kutoka katika hadeeth ya Abu Moosa Al-Ash'aree aliyesema: Rasoolullaah (Sallallaahu alayhi wasallam) amesema:"Imaam amewekwa ili afuatwe, kwahivyo akisema: "Allaahu Akbar nanyi mfuateni kwa kusema kama yeye na akianza kusoma, nyinyi nyamazeni." Vile vile akasema tena Ibn Katheer: Ibraaheem Ibn Muslim Al-Haajree amepokea kutoka kwa Abu Hurairah (Radhiallaahu 'anhu) aliyesema: "Wao (maswahaba) walikuwa wakizungumza na haliyakuwa wamo ndani ya swala, kwahivyo ilipoteremshwa aya hii ... waliamrishwa wawe kimya."

At-Tabaree akasimulia yakwamba Ibn Mas'ood amesema: "Tulikuwa tukipeana salamu miongoni mwetu haliyakuwa tumo ndani ya swala, kisha ikaja katika Qur'aan: Na isomwapo Qur'aan isikilizeni na nyamazeni"

At-Tabaree pia akasimulia, kutoka kwa Talhah Ibn 'Ubaidillaah yakuwa amesema: Niliwakuta 'Ubaid Ibn 'Umair na 'Attaa' Ibn Abee Rabah wakizungumza na hapo palikuwa na mtu akisoma Qur'aan, kwahivyo nikasema (kwa kuwaambia): "Hamutaki kuyasikiliza Makumbusho (Qur'aan) ili mupate ujira mulioahidiwa (kwa kutwi' amri)?" Walinitizama na kisha baadae wakaendelea na mazungumzo yao, nikarudia tena suali langu nao wakanitizama tena kisha wakaendelea na mazungumzo yao, nikaendelea kukariri suali langu kwa mara ya tatu hatimae wakaniangalia na kusema: "Jambo hilo ni katika swala peke yake: "Na isomwapo Qur'aan isikilizeni na nyamazeni ili mpate kurehemewa"

Vile vile imesimuliwa yakwamba Mujaahid amesema: "Hakuna pingamizi yoyote kwa mwenye kuzungumza wakati Qur'aan ikisomwa ikiwa sio ndani ya swala." Sa'eed Ibn Jubayr, Ad-Dahhaak, Ibraheem an-Nakhaee, Qataadah, Ash-Sha'bee, As-Suddee na Abdul-Rahmaan Ibn Zaid Ibn Aslam [1] wote hao wameafikiana yakwamba aya hii inahusiana na kuzungumza wakati wa swala peke yake. Imesimuliwa kutoka kwa Mujaahid kuwa alisema yakwamba aya hii inahusiana na swala na Khutbah ya Ijumaa, na ilivyosimuliwa na Sa'eed Ibn Jubayr yakwamba alisema, kuhusiana na aya hii, maana yake ni kuwa kimya kwenye Swala za faradhi, zikiwemo swala mbili za 'Idd na katika siku ya Ijumaa, pindi Imaam anaposoma Qur'aan kwa sauti kubwa. Haya ndiyo maoni yaliyopendekezwa na At-Tabaree. Ni muhimu hapa kutaja yakwamba, Mtume (Sallallaahu 'alayhi wasallam) aliposema: "Hana swala yule ambae hakuisoma (Soorat) al-Faatihah." (imepokelewa na Bukhaaree na Muslim). Hadeeth hii inapasa kueleweka kwa ufafanuzi wa hadeeth nyengine iliyo saheeh ambayo iliyofutilia mbali visomo vyote vilivyo kwenye Swala za usomaji kwa sauti kubwa ukiwa nyuma ya Imaam.

Ikasimuliwa kutoka kwa Abu-Hurairah (Radhiallaahu 'anhu) yakwamba Mtume (Sallallaahu 'alayhi wasallam), alipomaliza kusoma kwenye swala ya sauti kubwa (swala ya jahr) aliuliza: "Alikuwa mmoja wenu akisoma na mimi hivi sasa?" Bwana mmoja Akajibu: "Naam, ni mimi hapa, Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu!" Akasema: "Kwa hakika, nimehisi kama kuna kitu kinanikera?" Hapo basi, [Abu Hurairah (Radhiallaahu 'anhu)] akasema:

"Kuanzia hapo watu wakakoma kusoma pamoja na Mtume (Sallallaahu 'alayhi wasallam) pindi alipokuwa akisoma katika swala za jahr za sauti kubwa, baada ya kuyasikia maneno hayo kutoka kwake (lakini walikuwa wakisoma kwa sauti ya chini (kimya) katika swala ambazo Imaam hakuwa akisoma kwa sauti kubwa." (Yamepokewa maneno hayo na Maalik, Al-Humaidi, Bukhaaree katika kijitabu chake kidogo, Abu Dawood na wengineo).

Amma kuhusu swala za kimya, wajibu umesimama vilevile wa kuisoma Soorat Al-Faatihah katika kila rakaa'ah. Akasema Jaabir:

"Tulikuwa tukisoma nyuma ya Imaam katika swala za Adh-Dhuhr, na Al-'Asr: Soorat Al-Faatihah na Soorah nyengine katika rakaa'ah mbili za mwanzo na Soorat Al-Faatihah katika rakaa'ah mbili za mwisho." (Imepokewa na Ibn Maajah).

Kumbukumbu

[1] Hao wote waliotajwa ni wanavyuoni mashuhuri wa Ki-Islamu kutoka mwanzoni mwa karne za Uislamu.