Jitahadhari na (watu wa) Surooree!
Imetayarishwa Na: Sheikh Muqbil Ibn Haadee Al-Waadi'ee
Imefasiriwa Na: Abu Farida Muhammad A Basawad
Asili: Kitabu cha Tuhfat-ul-Mujeeb 'alaa As'ilat-il-Haadir wal-Ghareeb (uk. 179-185) ambacho ni kitabu kilichokusanya baadhi ya Fataawaa zake.

Bismillaahir Rahmaanir Raheem

Suali: Ni kina nani (watu wa) Surooree na ni zipi alama zao za kuwatambua. Kuwepo kwao ni uhakika au ni dhana za watu tu?
Jawabu: Sifa njema zote ni zenye kumthubutukia Allaah, Mola wa walimwengu na swala na salamu Zake zimshukie mtume Wake, Muhammad, ahli zake na maswahaba zake. Nashuhudia yakwamba hapana mola anaestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah - peke Yake na Asokuwa na mshirika. Na nashuhudia yakwamba Muhammad ni mtumwa Wake na mjumbe. Amma ba'd:
U-Surooree ni kujinasibisha na ndugu Muhammad Suroor Zayn-ul-'Aabideen. Alikuwa akiishi katika nchi ya Kuwait ambapo alikuwa akiandika baadhi ya vitabu vizuri vya kubainisha Imani za Shee'ah, pamoja na vitabu vyengine. Kisha akasafiri kuelekea nchini Ujerumani (Germany) na hatimae kumalizikia Uingereza (England) ambapo ndipo alipopafanya kuwa makao yake. Hapo akaanzisha jarida liitwalo "Al-Bayaan" ambalo lililotuvutia mno. Kisha akaanzisha Jarida jengine na akaliita "As-Sunnah" ambalo pia likatuvutia na kizidi kutufurahisha mpaka Tukasema: "Hili ndilo jawabu tulokuwa tukilisubiri kwa muda mrefu." Na baadhi ya ndugu zetu wakalisifu Jarida la "Al-Bayaan" ambalo hata sisi tulilisifu hapo awali, kwa kusema: "Hakuna mfano wake." Lakini hali za (watu wa) Hizbee ni kwamba kwanza hulingania katika Qur'aan na Sunnah mpaka wakajifungamanisha na nyoyo za watu na mara nguvu zao huzidi. Ikiwadhihirikia wao yakwamba hawadhuriki na lawama za mtu yoyote, ndipo wanapoamua kujitokeza na mafunzo yao waziwazi pasi na kujali chochote.
Hili Jarida la "As-Sunnah" ambalo lililostahiki kuitwa "Al-Bid'ah", huwalingania watu wajieke mbali na Wanavyuoni na kuwalaumu yakwamba wao (Wanavyuoni) hawafai chochote, kazi zao ni kulipwa na Serikali na ni wajinga katika kuyafahamu matukio ya kilimwengu.
Lakini Alhamdulillaah, ukweli wa (watu wa) Surooree ulijitokeza uwanjani wazi wazi wakati wa vita vya Guba. Hizo ni katika Rehma za Allaah ('Azza wa jall). Nakumbuka wakati huwo niliposoma maneno fulani (kutoka katika jarida lao) ambamo walimshambulia Sheikh Al-Albaanee kwa sababu alitoa kanda ya tepu iitwayo: "Mapambano na Surooree." Kisha baada ya kurasa kadhaa wakamsifu Shaykh Ibn Baaz. Basi mimi nikatambua tu maana ya sifa ya aina hii - ili isije ikasemekana yakuwa: "Wanawashambulia Wanavyuoni!"
Masiku kadhaa baada ya Fatwa ya Sheikh Ibn Baaz kuhusiana na ruhusa ya kuweka mkataba na Mayahudi ilipotolewa, walimshambulia Sheikh Ibn Baaz. Kwa hakika ilikuwa ni hila kabambe iliyokusudiwa kuwaweka watu kando na Wanavyuoni! Na haya Majarida mawili "Al-Bayaan" na "As-Sunnah" yakawafahamisha watu yakwamba ilikuwa ni aula zaidi kwao kutafuta muelekeo kwa wale (watu wa) Salafi wanaofahamu vyema matukio ya kilimwengu huko Yemen kuhusu hali ya matatizo na balaa zilipotokea Yemen.
Basi mimi nasema: Enyi Masaakeen [1]...ni yupi huyo asojua hali za Waislamu? Bali, matatizo yote yanangojea patokee marekebisho ya hii hali tulonayo sasa.
Kwahivyo maafa yaliyowapata Waislamu, yakiwemo ukorofi, khofu, mateso, yote hayo, basi ni kwa ajili ya madhambi yetu. Akasema Allaah (Subhaanahu wata'aalah) (kama ilivyofasiriwa):
"Na Mwenyezi Mungu Anakupigieni mfano wa mji uliokuwa na amani na utulivu, riziki yake ikiujia kwa wingi kutoka kila mahali. Lakini ukazikufuru neema za Mwenyezi Mungu, kwahivyo Mwenyezi Mungu Akauvika vazi la njaa na khofu kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyafanya." [Soorah An-Nahl 16:112]
Kwahivyo tutakapokuwa tumeyagundua maradhi, hayo matibabu yake basi ni yapi? Akasema Allaah (Subhaanahu wata'aalah) (kama ilivyofasiriwa):
"Mwenyezi Mungu Amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na kufanya vitendo vizuri, kuwa Atawafanya makhalifa katika ardhi kama Alivyowafanya makhalifa wale waliokuwako kabla yao, na kwa yakini Atawasimamishia dini yao Aliyowapendelea, na Atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu, hawanishirikishi na chochote. Na watakaokufuru baada ya hayo; basi hao ndio wavunjao amri zetu." [Soorah An-Noor 24:55]
Kwahivyo ni madhambi ndiyo ambayo yaliyoleta udhalilifu kwa Waislamu. Na ni kujishughulisha kwao na riba, kuruhusu kwao kwa uzinifu katika nchi za Ki-Islamu na ufadhilishaji na kuwa radhi kwao na sheria zisizokuwa za Mwenyezi Mungu walizoekewa na maadui wa Uislamu, tuongeze ngapi katika orodha yetu... na kutoka nje pasi na Hijaab na kutojisitiri ipasavyo (kwa wanawake), na michanganyiko ya wake na waume katika mashule na vyuo vikuu.
Kwahivyo matibabu yaliyoko ni kuregea katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Muhammad (Sallallaahu 'alayhi wasallam), na kisha ni kwa kuregea kwa Wanavyuoni. Akasema Allaah (Subhaanahu wata'aalah) (kama ilivyofasiriwa):

Soma Ukurasa wa Pili (Endelea)