Suluhisho La Matatizo Ya Umma Huu
Na: Imaam Muhammad Naasir ud-Deen al-Albaanee
Asili: Manhaj ya Salafi
Imefasiriwa Na: Abufarida Muhammad A. Basawad

Bismillaahir Rahmaanir Raheem

Mwanachuoni mkubwa wa hadhith wa karne hii (ya ishirini), Sheikh Muhammad Naasir ud-Deen al-Albaani (rahimahullah) aliulizwa: "Ni kwa misingi ipi, ulimwengu wa leo wa ki-islamu unaweza ukaregeshwa katika hali yake ya upya?"

Nae akajibu: "Mimi naamini yakwamba riwaya zilizopokewa katika hadith zilizo sahih zinabainisha jawabu waziwazi kwa maswali kama hayo na mfano wake ambayo yaliyo kithiri kwenye zama zetu hizi. Nao ni msemo wake (S.A.W): 'Mutakapo jishughulisha na biashara za riba na kushikamana na mikiya ya ng'ombe, na mukaridhika na mambo ya ukulima (mashamba) na mukawachana na kupigana jihaad kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (Swt), basi Mwenyezi Mungu atawadhalilisha. Na hatowaondolea udhalilifu huo mpaka muregee kwenye dini yenu'".1

Kwahivyo kurudi katika dini, ndio msingi mkubwa . Hali hii pia imezungumzwa na Imam Maalik (rahimahullah) katika msemo wake unaostahiki kuhifadhiwa kwa wino wa dhahabu .Nae Amesema:"Yeyote aneanzisha katika Uislamu jambo la uzushi ,na akalidhania kuwa ni zuri ,basi huyo amedai yakwamba Mtume Muhammad(S.A.W) amefanya khiyana katika (amana ya kuufikiliza) ujumbe. Soma maneno ya Mwenyezi Mungu, Alietukuka na Mwenye Nguvu: "Leo nimekukamilishieni dini yenu, na kukutimizieni neema Yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe dini yenu."2
Kwahivyo, chochote ambacho hakikuwa (katika sehemu ya )dini siku hiyo, si (katika sehemu ya) dini leo hii. Na sehemu ya mwisho ya Umma huu hautorekebishika, isipokuwa kwa kile kilichourekebisha sehemu yake (umma huu) yakwanza.

Kwahivyo, kama ilivyokuwa hali ya waarabu wakati wa siku za ujinga (jaahilyya) haikurekebishwa mpaka alipokuja Mtume (S.A.W) na risala kutoka mbinguni (wahyi) ndipo wao walipoupata uongofu hapa duniani, ambao ndio utakaowaokoa kesho (Aakhera). Kuimarisha misingi ya hali njema ya Uislamu ulio bora kwenye zama zetu hizi, si jengine isipokuwa ni kuregea kwenye Qur'aan na Sunna.
Ingawaje, jambo hili lahitaji kutiliwa mkazo katika kulidhihirisha, kutokana na idadi kubwa ya mapote ya ki-islamu na vyama vilovyojitokeza kwenye majukwaa wakidai kuwa wapo juu ya njia ambayo jamii ya ki-islamu na utawala wa ki-islamu unaweza ukaanzishwa.

Tunajua sisi kutoka kwenye kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume Wake (S.A.W) yakwamba njia ya kuelekea katika kulitekeleza (lengo) hili ni moja tu, nalo ni lile ambalo Mwenyezi Mungu (Swt) Alolitaja pindi Aliposema: "Na kwa hakika hii ndio njia yangu iliyonyoka.Basi ifuateni wala msifuate njia nyengine, zikakutengeni mbali na njia Yake (Mwenyezi Mungu)"3.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) akawafafanulia maswahaba zake. Siku moja aliwachorea mstari ulionyoka kwenye ardhi na kisha akachora vistari vyengine vidogo pambizoni mwake. Kisha, muda ule-ule kilipokuwa kidole chake kitukufu kikisongea juu na chini ya ule mstari ulionyoka, aliisoma hiyo aya iliyopita . Kisha akawaonyesha vile vistari vidogo alivyochora mule pambizoni mwa ule mstari ulionyoka na akasema: "Hii ni njia ya Mwenyezi Mungu na hizi ni njia (nyengine).Katika kila kilele cha hizi njia (nyengine),kuna shetani anae-itisha watu kuelekea kwenye mwito huo."4

Juu ya hayo, Mwenyezi Mungu (Swt) ayakinisha kwenye aya nyengine, kama alivyosema katika aya iliyopita pamoja na maelezo ya Mtume (S.A.W) kama ilivyoelezwa kwenye hadith. Kwahivyo Akasema Mwenyezi Mungu (Swt):"Na atakaemwasi mtume baada ya kumdhihirikia uwongofu na akafuata njia isiyokuwa ya waumini tutamgeuza alikogeukia mwenyewe na tutamwingiza katika jahannam ;napo ni pahali pabaya kabisa pa mtu kurudia."5
Katika aya hii kuna hikma kubwa iliyofichamana, kwani Mwenyezi Mungu (Swt) , Aliekamilika, Amezifungamanisha "njia za waumini" na aliyokuja nayo Mtume(S.A.W). Vile-vile Mtume (S.A.W)akatuashiria nukta hii katika hadith kuhusu kugawanyika kwa umma na kuwa mapote. Kwahivyo, alipoulizwa kuhusu pote litakalo okoka, akajibu kwa kusema: "Ni lile ambalo (liloshikamana kwa yale) nilojitegemeza nayo mimi na maswahaba zangu leo." 6

Pana hikma gani pale Mwenyezi Mungu (Swt) kutaja "njia ya waumini" kwenye aya hii? Na pana maana gani kwa Mtume (S.A.W) kujiunganisha yeye na maswahaba zake kwenye hiyo hadith iliyopita?
Jawabu ni kwamba: Hawa maswahaba watukufu ndiwo waliozipokea hizo risala mbili (Qur'an na Sunna) kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W), na kupewa ufafanuzi wake na yeye Mtume (S.A.W) moja kwa moja, pasi na kuwepo mjumbe yeyote. Lakini, ilikuwaje hali ya walokuja baada yao? Hapana shaka yakwamba hali hii ni kama alivyosema Mtume (S.A.W): "Hakika, yule aliyeko huona jambo lisilo-onekana na asokuweko."7
Hii ndiyo sababu Imani (kuamini) ya Maswahaba wa kwanza ilikuwa thabiti zaidi kuliko ya wale walokuja baada yao. Na hivi ndivyo alivyotueleza mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) katika hadithi mutawaatir: "Bora ya watu ni karne yangu, kisha ni wale walokuja baada yao na kisha ni wale walokuja baada yao."8
Kulingana na hadithi hii Muislamu hafai kujitegemea yeye mwenyewe binafsi katika kuifahamu Qur'an na Sunna. Ni afadhali atafute usaidizi katika kuvifahamu vitu viwili hivyo kwa kutaraji msaada wa maswahaba watukufu, kwani ni wao walokuwa wapokezi wa Mtume (S.A.W), na wakafahamishwa wakati mwengine kwa kutamka, na wakati mwengine kwa vitendo na kwa wakati mwengine kuwaruhusu kwa kuwanyamazia.

Ukurasa wa Mwisho